Uwanja wa Mashairi

-->
ULIMWENGU WETU
1. Jina la mola ndo kambi,nami ninakimbilia,
Ili anipe ulumbi,wa vina kupangilia,
Kati ya tungo tutumbi,yangu isije ingia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
2. Kuna wetu ulimwengu,tuliojichagulia,
Una radha kama kungu,ndugu zangu nawambia,
Kwetu hakuna ukungu,giza tumelikimbia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
3. Tumerefushwa mikono,mgongo twajisugua,
Tunajilia vinono,ni supu kwa vitumbua,
Tunabalikiwa mno,kila tunapopumua,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
4. Tunairamba asali,hamu inapotujia,
Hatuitafuti mbali,ndani tumejijazia,
Hatutumii nauli,radha kuisafilia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
5. Tunakula wali nazi,kwa viungo miamia,
Tunkula kwa mchuzi,vizuri unonukia,
Tunashushia kwa ndizi,tunda tunalotumia
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
6. Twakuta ndani liwazo,moyo unapoumia,
Yakitujaa mawazo, faraja hukimbilia,
Vitokeapo vikwazo mola,anatukingia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
7. Ulimwengu wetu pepo,si kufuru naapia,
Wanaishi kama popo,humu wasioingia,
Nami nashika kiapo,humuhumu nitafia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
8. Ulimwengu wa maraha,si peke niloingia,
Hata bwana Mafutaha,huku amekimbilia,
Atembea kwa madaha,Kalindima akimbia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
9. Bwana makame wa Tanga,tunda kashajivunia,
Mkongwe Jamili Mwanga,mbona ameshaingia,
Mtekateka katinga,mama kanichukulia
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
10. Abidala wa msese,kakayo hajakwambia,
Mboga twaunga mawese,kwa nyanya na mabamia,
Fanya bidii unase,vitamu uje jilia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
11. Raisi Mwakitalima,huku kumemnogea,
Kila apatapo nema,heka ujiongezea,
Waone kina Ndatama,wanavyojinenepea,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
12. Hakika nusu ya dini,sisi tumejitwalia,
Kama nanyi mwatamani,basi ifateni njia,
Mje ingia kundini,pepo kuikaribia,
Huu ulimwengu wetu,una radha kemkem.
Mtunzi:Lutufu A. Mbanga(Utu busara) S.L.P 1 MOROGORO –O655133337-lutufumbanga@gmail.com

No comments:

Post a Comment